Mkutano wa 65 wa Jumuiya ya Mawaziri wa Afya wa Nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini ECSA umemalizika leo jijini hapa kwa nchi wanachama kukubaliana maazimio mbali mbali yanayolenga kutekeleza kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari, saratani, magonjwa ya moyo na ya mfumo wa hewa.
Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema makubaliano hayo yamelenga kuimarisha na kuboresha sekta hiyo na afya ya wananchi kwa ujumla.
Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa wamekubaliana pia kuongeza uwajibikaji kwenye afya ya mama na mtoto ili kuepusha vifo vya mama na mtoto vinavyotokana na uzazi.
“Tumekubaliana kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza tumegundua katika nchi hizo magonjwa yanayoongoza ni pamoja na kisukari, saratani, magonjwa ya moyo na ya mfumo wa hewa” alisema Waziri Ummy.
Kwa mujibu wa Waziri Ummy amesema kuwa Suala lingine walilokubaliana ni kutilia mkazo suala la heshima kwa wajawazito kwa sababu mawaziri wameshauri pia Tanzania kukitambua Chuo cha Upasuaji cha Afrika Mashariki, Kati na Kusini.
Waziri Ummy ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, amesema wamkubaliana wamekubaliana pia kuimarisha ushirikiano na ulinzi katika maeneo ya mipaka.
“Kwa sababu nchi zina mipaka lakini magonjwa hayana mipaka tukiimarisha itasaidia kuondoa na kudhibiti uwezekano wa magonjwa hasa ya mlipuko kuenea ikiwemo Zika, Ebola, Dengue, Chikungunya na mengineyo,” alisema Waziri Ummy.
Pamoja na mambo mengine, Waziri Ummy amesema pia wamekubaliana kuimarisha masuala ya utawala kwamba kila mmoja ana wajibu kwa nafasi yake kwani sekta ya afya ni mtambuka.
“Tumeona kuna umuhimu mkubwa wa kushirikisha sekta zingine ikiwamo kilimo, maji, elimu, utumishi, mazingira zinahusika kwa ukaribu na masuala ya Afya” alisema Waziri Ummy.
Aidha Waziri Ummy amesema kuwa azimio la saba walilokubaliana katika mkutano huo ni kuweka mkakati wa pamoja kukabiliana na magonjwa akitolea mfano nchi ya Uganda ambao wamepata ugonjwa wa Marbugy unaofanana dalili na ugonjwa wa Ebola.
Mkutano huo wa kujadili masuala mbalimbali ya afya yalijumuisha nchi 9 kutoka Nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini ECSA umefanyika nchini Tanzania kwa siku tatu.







Post a Comment