Kamati ya Bunge ya Miundombinu imeeleza kuridhishwa kwake na ujenzi wa Barabara, Kivuko na uwanja wa ndege mkoani Mwanza na kusisitiza hali hiyo ikiendelea itawezesha Serikali kupata huduma zinazowiana na thamani ya fedha.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Moshi Sulemani Kakoso amesema kamati yake imeridhika kwa hatua zilizofikiwa katika ujenzi wa barabara ya Usagara-Kisesa KM 16.9, ujenzi wa MV misungwi II na upanuzi na ukarabati wa uwanja wa ndege wa Mwanza.
“Hakikisheni jengo la abiria lenye hadhi ya kimataifa linajengwa haraka katika uwanja wa ndege wa Mwanza ili kuwiana na urefu wa uwanja huu na hivyo kuvutia ndege nyingi katika ukanda wa Afrika Mashariki kutua Mwanza”, amesema Mhe. Kakoso.
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Hawa Mchafu ameitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), kuharakisha ujenzi wa uzio katika uwanja wa Mwanza ili kurahisisha huduma za usafi, utunzaji wa mazingira na usalama wakati wote.
Nae mjumbe wa kamati hiyo Mhe. Suzan Kiwanga amewataka wasimamizi wa miradi ya ujenzi nchini kuhakikisha wanatoa fursa za ajira kwa wanawake pale inapoonekana wana sifa za kufanya kazi husika ili kukuza uchumi wa jamii na kuhamasisha wanafunzi wa kike kusoma masomo ya sayansi na uhandisi.
Akizungumza kwa niaba ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anaeshughulikia (sekta ya ujenzi), Mhe. Elias John Kwandikwa amesema Serikali itaendelea kuhakikisha barabara na viwanja vya ndege vinajengwa kwa muda mfupi ili kuokoa gharama na pale itakapohitajika kulipa fidia kwa wananchi Serikali haitamuonea mtu.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea na sera ya kuwawezesha wakandarasi wazalendo ili kuwajengea uwezo katika ujenzi wa miradi ya kati na mikubwa ili kukuza uchumi wa nchi.
Kamati ya Bunge ya Miundombinu iko katika ziara ya kutembelea miundombinu inayosimamiwa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano katika mikoa ya Singida, Tabora, Shinyanga, Simiyu, Mwanza, na Mara.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano







Post a Comment